Saturday, March 30, 2013

SIKU YA TAIFA YA KUPANDA MITI 2013 KUADHIMISHWA KITAIFA MKOANI MOROGORO

Tarehe Mosi Aprili, kila mwaka ni Siku ya Taifa ya Kupanda Miti, hivyo kila mwananchi anatakiwa kupanda miti siku hiyo. Hata hivyo, kama ilivyo kawaida, kila Mkoa umechagua siku yake ya kupanda miti mingi kufuatana na majira ya mvua katika Mkoa husika. Mwaka huu Siku ya Taifa ya Kupanda Miti itaadhimishwa katika ngazi ya kitaifa katika Mkoa wa Morogoro ambapo upandaji miti utafanyika kwa wingi tarehe 3 Aprili kuzunguka bwawa la Mindu ambalo liko ndani ya ardhi inayomilikiwa na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine. Bwawa la Mindu ambalo liko umbali wa Kilomita 5 kutoka mjini Morogoro ndilo linalotoa maji yanayotumika mjini humo. Hivyo miti itakayopandwa itachangia katika kuhifadhi maji ya bwawa hilo. Wananchi wanaoishi karibuna bwawa hilo la Mindu, pamoja na jumuiya ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine watapanda jumla ya miche 2,300 siku hiyo ya maadhimisho . Nchini kote inakadiriwa kuwa jumla ya miti milioni 160 itapandwa na wananchi katika msimu wa kupanda miti mwaka huu.Kila Mwananchi anatakiwa kupanda Miti, au kutenga eneo ambalo miti itajiotea yenyewe na kutunzwa. Aina hii ya kupanda miti inayojulikana kama ngitili mkoani Shinyanga imeharakisha uongoaji wa maeneo ambayo hayakuwa na miti mkoani humo. Kaulimbiu ya mwaka huu ni:
MISITU NI UHAI. PANDA MITI KWANZA NDIPO UKATE MTI.
[MWISHO]
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
29 Machi 2013


TFSA-GS
Salim Shaaban Adha

No comments: